Hits 70190 | 3 online
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Dk.Mwinyi Talib Haji kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Dk. Mwinyi Talib Haji kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika leo Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Viongozi wa Idara Maalum za SMZ , viongozi wa serikali pamoja na wanafamilia.
Rais Dk. Mwinyi amemuapisha Mwanasheria huyo baada ya kumteua Novemba 3, mwaka huu kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu Nambari 55 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Haji alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.