Hits 70167 | 3 online
Wizara ya Katiba na Sheria Pemba yawapa mafunzo ya matumizi ya takwimu watendaji.
Maafisa Mipango, Utumishi na wanaohusika na takwimu waliopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria Pemba, wametahadharishwa kukusanya, kutumia, kuchambua na kutoa takwimu kwa mujibu wa miono yao pekee, kwani kufanya hivyo, hupelekea hata kuilisha serikali kuu takwimu zinazolega lega.
Kauli hiyo, imetolewa na Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Mattari Zahor Massoud, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa watendaji hao, yaliofanyika ukumbi wa wizara hiyo, Gombani nje kidogo ya mji wa Chakechake.
Alisema, takwimu ndio uti wa mgongo na roho ya serikali katika kukamilisha na kutengeneza mipango ya maendeleo ya kila siku, hivyo kama watajaribu kupeleka takwimu zisizo kuwa za uhakika kwa kutumia uzoefu wao pekee, wanaweza kuharibu mipango hiyo.
Mdhamini huyo alisema, suala la takwimu halihitaji ukusanyaji, uchambuzi na mtumizi kwa muhisika kutumia uzoefu pekee, bali jambo la kuzingatia ni uhalisia wa kila jambo.
Alieleza kuwa, hakuna namna yoyote ile katika ukusanyaji wa takwimu, bali njia pekee ni kutumia weledi na taaluma ya ukusanyaji wa takwimu, ili zinapopelekwa serikali kuu ziweza kutoa majibu sahihi.
“Sisi ndio chanzo kikuu cha ukusanyaji wa takwimu kuu za nchi, hivyo kama tutakusanya na kuzichambua kwa kutumia uzoefu wetu pekee, tujue kuwa tutaitia hasara na mwelekeo usio mzuri wa serikali na washirika wake,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Afisa Mdhamini huyo wa Katiba na Sheria Pemba, Mattar Zahoro Massoud, aliwataka watendaji hao waliochini yake, kuhakikisha wanakuwa makini kwenye mafunzo hayo, ili watakapomaliza wawe wakusanyaji, watumiaji, na wachambuzi bora wa takwimu.
Akiwasilisha mada ya maana na umuhimu wa matumizi ya takwimu, Kaimu afisa mipango wa wizara hiyo, Mussa Alei alisema, ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali, inategemea sana kupata takwimu sahihi, kuanzia ngazi ya Idara hadi wizara husika.
Alisema, hilo linaweza kufanikishwa, iwapo wakuu wa vitengo watakusanya takwimu sahihi na kuwa na uchambuzi unaokubalika kwa mujibu wa masharti na miongozo ya utumiaji wa takwimu.
Alisema, matumizi sahihi ya takwimu daima, hutokana na ukusanyaji sahihi kwa mujibu wa vigezo na masharti ya utumiaji wa takwimu, kama taratibu zinavyoeleza.
“Ili uwe na matumizi au uchambuzi sahihi wa takwimu, kwanza zianzie kwenye namna ya utafutaji, ukusanyaji hapo kisha matumizi yake yanaweza kuwa ya uhakika,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, aliwataka wakuu hao wa maidara kuhakikisha wanazitunza na kuzihifadhi vyema takwimu, ili iwe rahisi katika upatikanaji wake kwa wakati.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya ukumbi huyo Afisa Mipango wa Kamisheni ya wakfu na mali ya amana Pemba, Salma Omar Ali alisema mafunzo hayo ni chachu ya ukusanyaji wa takwimu .
Alisema anatarajia kufanya kazi zake kwa ufanisi, huku akizingatia umuhimu na ubora wa ukusanyaji wa takwimu katika Idara yake.
Nae Afisa Utumishi wa ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kisiwani Pemba, Rashid Ali Mussa, alisema moja ya jambo alilojifunza kwenye mafunzo hayo ni thamani ya ukusanyaji na matumizi ta takwimu sahihi.
Alisema hayo ni mafunzo yake ya kwanza, hivyo kwenye eneo la takwimu walikuwa wakikusaya, kuchambua na kuzitumia kwa kubahatisha, jambo ambalo anadhani sio zuri.
Hata hivyo, Afisa Utumishi huyo, aliwataka wenye mamlaka kuhakikisha hawazifichi takwimu hasa kwa waandishi wa habari pale wanapozihitaji, kwani ni njia moja ya kuionyesha jamii kazi zinazofanywa na serikali.
“Kuficha takwimu sio jambo zuri, sasa kama wapo wenye tabia hiyo ni kuhakikisha wanaiacha maana, takwimu ndio njia halisi katika kuhakikisha ufanikisha wa miradi,’’alieleza.
Katika mafunzo hayo ya siku moja, Idara mbali mbali zilizochini ya wizara ya Katiba na Sheria kama vile ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, mahakama, Kamisheni ya wakfu na mali ya amana ofisi kuu zimeshiriki.