Hits 70166 | 3 online
Mrajis wa Mahakama Zanzibar Mhe Mohamed Ali Mohamed akifunguwa mkutano kujadili Kanuni ya Sheria ya Mahakama ya Kadhi Zanzibar.
Nia ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuona kuwa haki za mtoto zinalindwa na zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria hivyo ni vyema sheria zinazotungwa kuhakikisha zinatungiwa kanuni ili ziweze kutekelezeka
Mrajis Mkuu wa mahakama Zanzibar Mhe Mohamed Ali Mohamed ameyasema hayo wakati akifunguwa mkutano wa wadau wa kujadili kanuni za Mahakama ya kadhi uliowakutanisha Makadhi wa wilaya zote Unguja na Pemba pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya sheria
Mhe Mohamed amesema sheria ambayo haijatungiwa kanuni utekelezaji wake unakuwa mgumu hivyo kuwepo kwa kanuni kutasaidia kutekelezeka kwa sheria no 9 ya Mahakama ya kadhi ya 2007 na kuwaomba makadhi na washiriki wa mkutano huo kuzipitia kwa umakini kanuni zilizotayarishwa ili kuweza kupata kanuni ambayo itaweza kutekelezeka
Aidha Mohamed amewataka makadhi hao kuangalia kwa makini viambatanisho vya kanuni ili kusiwepo na kukinzana kwa sheria kwa vile taratibu zinazotumika katika Mahakama ya watoto na Mahakama ya Kadhi mara nyingi huwa zinafungana
“nawaomba makadhi wenyewe mtowe michango endelevu kwa vile ndio Wahusika Wakuu wakuitumia kanuni hizi za mwenendo wa Mahakama ya kadhi ili hatimae tuwe na sheria inayotekelezeka na kuondoa mgongano uliopo kwani sote tunaelewa namna ya haki za watoto na changamoto zake”alisisitiza Mrajis
Nae mwakilishi wa shirika la umoja wa Mataifa la kusaidia watoto UNICEF kutoka Zanzibar ndugu Ahmeid Rashid Ali amesema Mahakama ya kadhi ndio kimbilio la wazanzibari walio wengi hasa kwa kesi zinahusiana na ndoa , malezi na talaka jambo ambalo limepelekea UNICEF kuona ipo haja ya kushirikiana na Serikali kupitia Mahakama kusaidia katika kutengeneza miongozo ya Mahakama ya Kadhi
Mwakilishi huyo kupitia UNICEF amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuisaidia mafunzo kwa makadhi, kutafsiri kanuni kwa lugha nzuri na nyepesi pamoja na kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri, wanakuwa vizuri, wanapata haki zao na stahili kama inavyotakiwa
Nae mshauri mwelekezi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ndugu Ali Hassan Ali amesema makadhi wanalo jukumu kubwa la kuelewa vifungu vya sheria hivyo ni vyema wakatenga muda wa kujisomea ili waweze kivifahamu na kuvifanyia kazi kwa uadilifu vifungu vya sheria
Pia ameshauri kuwa ni vyema katika Mahakama za Kadhi kuwepo na maafisa ustawi tokea mwanzo wa kesi inapoanza kusikilizwa hadi mwisho kwani tayari wanaelimu na uelewa mpana ambao utasaidia sana mtoto kupata haki yake ya msingi
Kwa upande wa watu wenye ulemavu mshauri mwelekezi huyo amesema watoto wenye ulemavu na wagonjwa wa akili wanahitaji matunzo hata kama watakuwa wamepitiliza umri wao wa miaka 18 na kusisistiza kuwa haki ya mtoto ziendane na utamaduni wetu na silka asili ambao hautaleta athari katika kutekeleza majukumu ya mtoto
Mtoto anaesoma anatakiwa apewe matunzo na wazazi wake hata kama atakuwa amepitiliza umri wa miaka 18 kwa vile bado atakuwa anaitegemea familia “mahakama itaamuru mzazi kumhudumia mtoto kama itakavyoelezwa katika kifungu cha sheria
Nao washiriki wa mkutano huo wameomba kiwepo kwa kifungu cha adhabu cha kuwekwa ndani kwa mzazi atakaemnyima matunzo mtoto wake baada ya kuachana hii itasaidia wazazi kutokwepa majukumu na wajibu wao kwa mtoto
“Wazanzibari tuna utamaduni wetu wa kipekee wa kusaidiana na kupeana ushauri baba atakapowekwa ndani iwapo hatowi huduma zipo baadhi ya familia zitajitokeza kumchangia sio mbaya muhimu mtoto apewe huduma ambayo ndio haki yake ya msingi”
Mkutano huo ulihudhuriwa na Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji khamis , kadhi wa Rufaa Pemba na kufungwa na Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Hassan Ngwali ambapo amewasihi majaji kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao kila siku, kila mmoja apewe haki yake na kutoyafumbia macho yale yote yanawakwaza
Sheikh Ngwali amesema katika sheria ya kiilslamu kuna kur-ani na sunna ambao ndio muongozo na pia ulimwengu una sheria na kanuni yote haya yanatoa urahisi katika utekelezaji wa kazi zinazofanywa na makadhi na majaji hivyo ni wajibu kushikamana kuzidisha bidii ya kazi ili kila mmoja apate haki yake.