Hits 86474 | 2 online
ofisi ya mufti zanzibar imetakiwa kutafuta uwezekano wa kukifanya cheti cha mafunzo ya ndoa kuwa ni lazima kiwepo kabla ya kufungisha ndoa kama kilivyo kwa cheti cha upimaji wa vvu na ukimwi kwa sasa.
Ofisi ya Mufti Zanzibar imetakiwa kutafuta uwezekano wa kukifanya cheti cha mafunzo ya ndoa kuwa ni lazima kiwepo kabla ya kufungisha ndoa kama kilivyo kwa cheti cha upimaji wa vvu na ukimwi kwa sasa.
Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo ya ndoa ya awamu ya tano Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Wanawake Mh, Mgeni Hassan Juma amesema vyeti hivyo ni muhimu kwani vitasaidia kuwajua waliopata mafunzo na kuondosha kukithiri kwa talaka katika jamii.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasikitishwa sana na ongezeko la talaka nchini kwani linasababisha kukosekana kwa nguvu kazi ya taifa kwa vijana wengi kujiingiza katika vitendo viovu baada ya kukosa malezi ya pamoja ya wazazi wawili.
Aidha ameiomba Wizara ya Elimu Zanzibar kuingiza mafunzo ya ndoa katika mtaala wa elimu hasa katika somo la dini ili kuwapa uelewa mzuri pale wanapofikia uamuzi wa kuingia katika ndoa ili kuondoa tatizo la vijana wadogo kuachika na kusumbuka na watoto mitaani.
Ameiomba Ofisi ya Mufti Zanzibar kuhimiza na kushajihisha mashehe wa Wilaya kuanzisha madarasa ya mafunzo ya ndoa katika wilaya zote za Unguja na Pemba sambamba na kuitaka Ofisi hiyo kuwapa uelewa wazazi ili wasiwe chanzo cha uvunjifu wa ndoa.
Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa Zanzibar Bi, Mariyam Hamdani amesema mafunzo haya yamekuja katika wakati mzuri na linamchango mkubwa katika jamii na kuitaka Mfisi ya Mufti Zanzibar kuziangalia kwa makini sherehe za harusi hasa zile za upigaji wa madufu ili kulinda silka na maadili ya Mzanzibari.
Mkuu wa fatwa na utafiti ambae pia ni mwalimu mkuu wa mafunzo hayo Sh, Thabit Nouman Jongo akizungumza kwa niaba ya Katibu wa Mufti Zanzibar amewataka wanafunzi hao kuwa walimu wazuri katika jamii na kuwa mfano bora katika ndoa zao kwa kuyatekeleza kwa vitendo mafunzo waliyoyapata.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wanafunzi wenzake Nd, Ziada Suleiman Khamis ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Mufti kwa kuyaendeleza vyema mafunzo hayo na kuahidi kuwa kigezo bora katika jamii.