Hits 70163 | 3 online
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman amewataka watoa huduma za kisheria kufanyakazi kwa uadilifu na upendo mkubwa.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman amewataka watoa huduma za kisheria kufanyakazi kwa uadilifu na upendo mkubwa.
Aliwaeleza kuwa wajibu wao ni kuwasaidia wananchi wanaonyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na sio kukusanya fedha kutoka kwao.
Waziri Haroun alitoa maelekezo hayo katika Maadhimisho ya wiki ya Msaada wa Kisheria mwaka 2020 na Uzinduzi wa Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa lugha nyepesi pamoja na mfumo wa kuwasajili watoa huduma za msaada wa kisheria kwa njia ya kielektroniki katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni
Alisema wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria wengi wao ni wanyonge na wamejenga matumaini mapya ya kuwa wakombozi wa matatizo yanayowakabila.
‘’Nendeni mukatoe msaada wa kisheria, watoto wanadhulimiwa baada ya wazazi wao kufariki na wanawake wajane wanadhulumiwa haki zao, kuna udhalilishaji mkubwa,’’ Waziri Haroun aliwaeleza watoa huduma za Kisheria.
Aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizowekwa ndani ya Sheria hiyo ili wanaotekeseka waweze kupata haki zao.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman aliwasisitiza Wanasheria kujenga uzalendo katika kulinda Sheria za nchi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake anayostahiki kuipata.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg George Joseph Kazi alisema Serikali imeweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa msaada wa kisheria na ndio ikaanzishwa Idara maalum ya Msaada wa Kisheria ambayo iko chini ya Wizara hiyo.
Alisema Idara ya Msaada wa Kisheria ni mkombozi na nguvu imara ya kuwasaidia wananchi wanaodhulimiwa na kunyanyaswa ambapo amewashauri kuitumia Idara hio kikamilifu ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria Bi Hanifa Ramadhan Said aliwakumbusha watoa huduma za Kisheria kuhakikisha wanajisajili ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya Msaada wa Kisheria 2020 ni ‘Upatikanaji wa Msaada wa Kisheria ni nguzo imara kwa ustawi wa jamii.’