Head image
Govt. Logo

Hits 30385 |  2 online

     
Kamati ya Sheria, Utawala bora na Idara maalumu ya Baraza la Wawakilishi imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahakama Kuu Tunguu .
news phpto

Kamati ya Sheria, Utawala bora na Idara maalumu ya Baraza la Wawakilishi imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahakama Kuu Tunguu .

Hayo yameelezwa na Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Zulfa Mmaka Omar ambae wakati walipofanya ziara kuangalia ujenzi unaoendelea wa Mahakama Kuu ya kisasa Tunguu na baadhi ya Mahakama ikiwemo Mkokotoni na Mahonda pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji robo ya pili ya Oktoba – Disemba 2019 ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mhe Zulfa amesema hatua iliyofikiwa ni nzuri hivyo ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kuona taasisi zote zinazohusika zinashirikiana katika kurahisisha upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika ujenzi huo na kuweza kumaliza kwa wakati.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo na kukamilisha vipaumbele vya Serikali ambapo kati yake ni kukamilika Ujenzi wa Mahakama Kuu mpya Tunguu “macho ya Kamati hii Serikali na wananchi hivi sasa yanaangalia ujenzi wa Mahakama nasisitiza changamoto zilizopo zitatuliwe ili ujenzi ukamilike kwa wakati ”

Aidha ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuboresha majengo ya mahakama za mikoa na wilaya Unguja na Pemba kwa kuyafanyia ukarabati ili majengo hayo yaweze kuwa na hadhi za mahakama.

Nae Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mhe Khamis Juma Mwalim amesema changamoto zilizojitokeza hasa ya mchanga tayari zimeshapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo Maliasili zisizorejesheka na kuahidi kuendelea kutatua changamoto zitakazojitokeza ili azma ya Serikali iweze kufikiwa ili jengo hilo liweze kukamilika kwa wakati.

Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar ndg Mohamed Ali Mohamed amempongeza Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein na Serikali kwa ujumla kwa kujenga na kufungua majengo mapya ikiwemo kufanyika kwa matengenezo makubwa ya majengo mbali mbali ya mahakama Unguja na Pemba na kuahidi kuyaenzi na kuendeleza ukarabati wa majengo yaliyobaki.

“Tunakusudia kuzikarabati upya Mahakama zetu zote na kurudisha haiba na uasili hatutaondosha au kubadilisha bali tunazingatia vigezo na umuhimu wa kuenzi majengo yetu uimara na utekelezaji mzuri wa majukumu ya kazi kwa watendaji wetu ” alisisitiza Mrajis wa Mahakama Kuu

Mhandisi wa Mahakama Kuu Tunguu ndg Mussa Ali Hamad ameahidi jengo hilo kumalizika kwa wakati kwani changamoto kubwa zilizokua zikizorotesha ujenzi huo tayari zimesha tatuliwa.

Wakitoa michango yao wakati wa majumuisho baadhi ya wanakamati Kupitia Wizara wameomba kuwepo kwa mashirikiano kati ya waendesha mashtaka wapelelezi na Polisi ili waende sambamba na utowaji wa haki

Kwa upande mwengine wameitaka Ofisi ya Mufti kuandaa muongozo wenye kufuata utaratibu maalum wa ufundishaji kwa wanafunzi wa madrasa za kur-ani badala ya utaratibu uliopo sasa kila mwalim ama Ustadh kufundisha vile wanavohisi inafaa

Kamati imehimiza kuungana pamoja kwa taasisi za Serikali hasa zile ambazo zitakuwa zinategemeana mahitaji ili kurahisisha upatikanaji wa mahitaji ya lazima katika miradi ya maendeleo jambo ambalo litawezesha kukamilika kwa wakati kwa miradi iliyopangwa

Ujenzi wa Mahakama ya Tunguu umeanza rasmi tarehe 21 Octoba 20019 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na jengo hilo litakuwa la ghorofa nne

Huduma za Tehama

Barua Pepe Msaada wa kisheria

Sisi

Mwanzo Kuhusu Sisi Idara Zetu

Viunga Muhimu

MAHAKAMA DPP WAKFU LRC SADC IKULU

Mawasiliano

Ofisi Kuu
S.L.P 772, Mazizini, Zanzibar
Tel.: +255(24)2234683 Mhe WaziriTel.: +255 (24)2234684 Katibu Mkuu,
Fax: +255 (24)2234689
Email: info@sheriasmz.go.tz